Mtoto Nuru Mohamedi (7) ameuawa kikatili na kisha mwili wake kutelekezwa kwenye nyumba ambayo haijakamilika ujenzi iliyo Majohe Kichangani jijini Dar.
Tukio hilo, ambalo limezua hofu
na huzuni kwa wakazi wa mtaa huo, lilibainika jana baada ya kupatikana
kwa maiti ya mtoto huyo ambaye kabla ya mauti kumkuta alikuwa amepotea
katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 6.
Akisimulia
tukio hilo kwa tabu huku akilia kwa huzuni, mama mzazi wa mtoto huyo,
Sauda Ally alisema Alhamisi iliyopita saa 1:00 usiku mtoto wake alikuwa
akicheza nje ya nyumba yao pamoja na watoto wengine wawili.
“Baadaye
akaja mtoto wa jirani aitwaye Dula, akaniambia Nuru amekwenda na babu
mmoja alimwambia amsindikize dukani, nilinyanyuka haraka na kutoka nje
na kuanza kumwita, lakini hakuitika,” alisema.
Alisema
baada ya kuona hali hiyo alikimbia hadi dukani alikoelekezwa kuwa
mwanaye amekwenda, lakini hakumwona hivyo aliamua kuomba msaada kwa
majirani na taarifa zilipelekwa katika msikiti wa karibu kwa ajili ya
kutangazwa na kisha waliendelea kutoa taarifa hizo kituo cha polisi cha
Gongo la Mboto.
Alisema mtoto wake alitafutwa bila mafanikio kwa siku sita.
Alisema,
jana asubuhi mmoja wa wapangaji wake alipokea simu kutoka kwa jirani
yake anayeishi eneo la Kwa Mkandawile kwamba kuna maiti ya mtoto
imeonekana katika maeneo hayo na kwamba huenda akawa ni mtoto wake.
Hata
hivyo, Sauda alishindwa kuelezea zaidi mkasa huo na mama mkubwa wa
marehemu, Rehema Ally alisema kuwa baada ya simu hiyo waliondoka mara
moja kwenda eneo la tukio.
“Tuliona maiti ya mtoto ikiwa imefukiwa kwa matofali na sehemu ya kichwa ikiwa imebaki nje”.
“Kwa
kweli hali tuliyoikuta ilikuwa inatisha. Alikuwa amefunikwa kwa
matofali, upande wa kisogoni tu ndiyo ulikuwa ukionekana. Tulitoa
taarifa polisi na walipofika, waliinyanyua na ndipo tulipothibitisha
maiti ile ilikuwa ya Nuru na alikuwa amevuliwa nguo zote.”
Alisema watekelezaji wa tukio hilo walifanya ukatili wa hali ya
juu, kwani baada ya uchunguzi wa daktari ilibainika kuwa na majeraha
katika sehemu ya paja, lililokuwa na tundu lililofunikwa kwa plasta na
kisogoni ilionekana amepigwa na kitu kama jiwe.
Alisema
anasikitishwa na kitendo cha kuuawa kinyama na kudhalilishwa
alichofanyiwa mtoto wao, kwani kinaonyesha kushuka kwa hali ya usalama
wa watoto na kuitaka polisi kuhakikisha inachunguza kwa undani taarifa
za utekaji watoto na si kuzipuuzia.
Aliongeza kuwa maiti ya mtoto wao walitarajia kuizika jana baada ya taratibu za kipolisi kukamilika.
Hata
hivyo, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walipeleka lawama zao kwa polisi
kwa kukanusha taarifa za utekaji watoto pasipo kuzifanyia uchunguzi wa
kina.
Mkazi mwingine, Zena Ramadhani alisema kupotea
kwa Nuru ni tukio la pili kwa eneo hilo ndani ya mwezi mmoja na mtoto wa
kwanza kupotea hajaonekana hadi leo.
“Hivi sasa
tunaishi na watoto wetu kwa shaka, japo polisi wanasema hakuna utekaji
nyara, sisi kama wazazi hatukubaliani na hilo kwa sababu nimeshuhudia na
hili ni tukio la pili. Sasa utaniambiaje kuwa taarifa hizo ni za
uongo.”
Alipotafutwa Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Suleiman Kova alikataa kuzungumza moja kwa moja na kusema
atafutwe Kamanda wa Ilala, Mary Nzuki.
Hata hivyo,
Kamanda Nzuki alipopigiwa simu zaidi ya mara tano hakupokea na hata
alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kuhusiana na tukio hilo, hakujibu.
Ustadhi
wa msikiti katika eneo hilo, Jumanne Hamis ambaye pia ni mwenyekiti wa
CCM Mtaa wa Kichangani, aliyetoa tangazo la kupotea kwa mtoto msikitini
kwa mara ya kwanza alisema amesikitishwa mno na taarifa za kifo cha
mtoto huyo.
“Kwa kweli siamini kilichotokea na kama kuna binadamu anayeweza kufanya jambo hilo kwa mtoto wa miaka saba.”
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
Mtoto aliyepotea auawa kikatili, maiti yaokotwa ndani ya Pagala
Reviewed by Unknown
on
12:44:00 AM
Rating: