Licha
ya kutoa ajira kwa maelfu ya vijana wa Kitanzania na pia kupunguza
tatizo la usafiri mijini litokanalo na foleni, usafiri wa pikipiki
maarufu kama 'bodaboda' umeendelea kuua watu kimyakimya na
kuwasababishia ulemavu wa kudumu maelfu ya manusura wa ajali za vyombo
hivyo kila uchao.
Uchunguzi
uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa mbali na vifo na ulemavu, bodaboda
zimeathiri pia utoaji wa huduma katika hospitali zinazopokea majeruhi wa
vyombo hivyo, kwani wodi zimefurika kupita kiasi na kusababisha
wagonjwa wengi kulala chini.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, ameiambia NIPASHE kuwa katika kipindi
cha mwaka 2013 peke yake, pikipiki 8,241 zilihusika katika ajali 6,831
na kusababisha vifo vya watu 1,098 na kuwajeruhi wengine 6,578; huku
baadhi yao wakiishia kupata ulemavu wa kudumu. Idadi hiyo ni sawa na
wastani wa vifo vya watu watatu kila uchao na majeruhi 18.
DAR, MORO, PWANI VINARA
Akieleza
zaidi, Kamanda Mpinga anasema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi
Agosti mwaka huu, pikipiki 3,998 zilihusika kwenye ajali 3,777 na
kusababisha vifo vya watu 608 na majeruhi 2,883.
Aidha, takwimu
za mikoa zinaonyesha kuwa jiji la Dar es Salaam ndilo linaloongoza kwa
kuwa na matukio ya ajali za bodaboda. Mwaka jana, bodaboda 3,970
zilihusika katika ajali 3,405 jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo
vya watu 172 na majeruhi 3,541.
Kadhalika, katika kipindi cha
Januari hadi Agosti mwaka huu, jiji la Dar es Salaam lilikuwa na ajali
1,687 zilizohusisha pikipiki 2,280 na kusababisha vifo vya watu 113 na
majeruhi 1,539.
Kamanda Mpinga anasema mkoa unaoshika nafasi ya
pili kwa ajali za bodaboda ni Morogoro; uliokuwa na ajali 657 na
kuhusisha pikipiki 866 zilizosababisha vifo 73 na majeruhi 557 kwa mwaka
2013
Mwaka
huu, kwa kipindi cha Januari hadi Agosti, Morogoro kulikuwa na ajali
191 zilizohusisha pikipiki 264 na kusababisha vifo vya watu 41 na
majeruhi 202.
Mpinga anautaja mkoa unaoshika nafasi ya tatu kuwa
ni Pwani, wenye matukio 428 ya ajali zilizohusisha pikipiki 589, vifo
vya watu 84 na majeruhi 466 kwa mwaka 2013, huku kwa kipindi cha Januari
hadi Agosti mwaka huu mkoa huo ukiwa na matukio 121 yaliyohusisha
pikipiki 164 na kusababisha vifo vya watu 40 na majeruhi 172.
Kilimanjaro
unashikilia nafasi ya nne katika janga hilo. Ulikuwa na ajali 372
zilizohusisha pikipiki 409 na kusababisha vifo vya watu 74 na majeruhi
343 kwa mwaka 2013.
Kuanzia
Januari hadi Agosti mwaka huu, mkoa huo ulikuwa na ajali 104
zilizohusisha pikipiki 121 na kusababisha vifo vya watu 22 na majeruhi
88.
Mikoa mingine na idadi ya ajali za bodaboda katika kipindi
cha mwaka 2013 kwenye mabano ni Ruvuma (213), Katavi (190), Arusha
(180), Manyara (154), Tabora (128), Dodoma (123), Rukwa (110), Mwanza
(96), Mbeya (90), Kigoma ( 82), Shinyanga (81) na Kanda Maalum ya
Tarime/Rorya ajali 80.
Mingine ni Mtwara (77), Lindi (59),
Singida (54), Geita (50), Kagera (43), Mara (42), Tanga (35), Njombe
(27) na Simiyu ikiwa na matukio machache zaidi ya ajali za bodaboda
yaliyoripotiwa Polisi baada ya kukumbwa na ajali 18 katika kipindi chote
cha mwaka 2013.
Akielezea kuhusu hatua zitakazosaidia kupunguza
zaidi ajali za bodaboda nchini, Mpinga anasema elimu ndiyo nguzo ya
kumaliza ajali za bodaboda na kwamba tangu mwaka 2010, wamekuwa wakitoa
elimu na wanaamini kuwa walau kiwango cha ajali za bodaboda kimekuwa
kikipungua.
Kamanda Mpinga anasema katika utafiti wao, wamebaini
vyanzo vya ajali nyingi ni makosa ya kibinadamu ambayo ni pamoja na
kutoheshimu sheria, mwendo wa kasi, ulevi wa madereva (ukiwamo wa
unywaji wa viroba kabla ya kuendesha), pikipiki kupakiza abiria wengi
zaidi ya uwezo wake maarufu kama mishkaki na madereva kutokuwa na leseni
zinazothibitisha kuwa na uwezo wa kutumia vyombo hivyo vya moto.
Anataja
vyanzo vingine kuwa ni ubovu wa miundombinu kama mashimo, utelezi na
kona kali barabarani na watumiaji kutovaa kofia ngumu (helmet) huchangia
kuongeza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za pikipiki.
REKODI YAWEKWA MOI
Uchunguzi
wa NIPASHE umebaini kuwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) peke yake
hupokea wastani wa majeruhi 77 kwa wiki wanaotokana na ajali za
bodaboda, hiyo ikiwa ni sawa na wastani wa majeruhi 11 kwa siku.
Dk.
Mwanga Joseph wa Moi anasema asilimia 55 ya majeruhi wote wanaofikishwa
kwao kutokana na matukio ya ajali jijini Dar es Salaam huwa ni kutokana
na bodaboda.
Anasema wingi huo wa majeruhi wa bodaboda
husababisha mrundikano wa wagonjwa wodini kiasi cha kuzidi idadi ya
vitanda na hivyo wengi hulazimika kulala chini.
Anasema
licha ya changamoto zilizopo sasa, wao wanaendelea kutekeleza wajibu
wao wa kutoa huduma na wanaamini kuwa ufumbuzi wa tatizo la mrundikano
uliopo sasa Muhimbili ni kuwa na matawi zaidi ya Moi kuanzia ngazi ya
mkoa na wilaya ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaofikishwa hapo kila
uchao.
Msemaji wa Moi, Patrick Mvungi, anasema kwa mwezi mmoja,
wagonjwa wa ajali ni 600 na kati yao, 330 sawa na asilimia 55, ni wa
ajali za bodaboda.
Mvungi anasema kuwa licha ya majeruhi wa
pikipiki kuwa wengi kiasi cha kuzidi uwezo wa wodi zao, bado
wanapowapokea huwachukulia kuwa ni sawa na majeruhi wengine na wala
hawawatengi kwenye wodi maalum kama ambavyo imekuwa ikivumishwa na
baadhi ya watu.
" Kuna uvumi kuwa (Moi) tumetenga wodi kwa ajili
ya majeruhi wa ajali za pikipiki... (hili) siyo kweli. Hata viongozi wa
waendesha pikipiki wa Temeke kupitia umoja wao walishafika kuuliza hilo,
tukawahakikishia kwamba majeruhi wote wanalazwa kwenye wodi moja bila
kubaguliwa na hivyo hakuna sehemu maalum kwa ajili yao," alisema.
Akieleza
zaidi, Mvungi anasema kuwa kwa ujumla hali siyo nzuri kutokana na
msongamano wa wagonjwa unaotokana na ajali nyingi za bodaboda.
"Wodi
ina uwezo wa kulaza wagonjwa 33 kwa maana ya vitanda vilivyopo, lakini
wagonjwa huongezeka na kufikia 90. Hali hii siyo nzuri. Tunalazimika
kuweka magodoro chini na kuwapa huduma kwa sababu sisi ni hospitali ya
umma, hatuwezi kumkataa mgonjwa anapofikishwa (kwetu) akiwa katika hali
yoyote ile," anasema.
Mvungi anasema kuwa mbali na mipango
mingine kadhaa waliyo nayo, lakini njia mojawapo ya kukabiliana na
changamoto ya mrundikano wa wagonjwa kwenye wodi zao ni kukamilika kwa
jengo la ghorofa saba hivi karibuni litakalokuwa na vitanda 380 na vifaa
vingine vingi vya kisasa.
"Licha ya hali ngumu iliyopo sasa, (sisi) tunaendelea kuwa taasisi bora inayotoa huduma kwa wagonjwa," anasema.
"Ndani
ya jengo hilo tutaboresha zaidi kwa kuwa tunatumia mfumo wa kompyuta na
kuachana na mafaili (ya makaratasi) katika kuhifadhi taarifa za
mgonjwa. Madaktari watakuwa na uwezo wa kuwasiliana na wenzao waliopo
nje katika uboreshaji wa huduma za afya," anasema na kuongeza kuwa
taasisi yao imetunukiwa cheti cha ubora Afrika Mashariki.
GHARAMA BADO NAFUU
Mvungi
anasema gharama za upasuaji ni Sh. 200,000 na za kupokewa kwa huduma za
awali ni Sh. 50,000, hiyo ikiwa ni nusu ya gharama halisi.
Anasema
katika ajali nyingi za bodaboda, majeruhi huvunjika mfupa mrefu wa mguu
ambao hutakiwa kuwekwa vifaa maalum vinavyouzwa nje ya nchi kwa dola
300 za Marekani (Sh. 480,000).
Anasema kwa ujumla, gharama
anazolipa mgonjwa ni ndogo kwa kuwa serikali hutoa ruzuku na kwamba, kwa
kawaida huwa kuna wagonjwa wa aina mbili; ambao ni wanaolipiwa na Moi
baada ya kushindwa kumudu na wengine wanaojilipia wenyewe.
MAJERUHI KUTELEKEZWA WODINI
Anaongeza
kuwa majeruhi wengi wa bodaboda hawana uwezo wa kumudu gharama za
matibabu na kwamba umoja wao (waendesha bodaboda) huonekana siku
wanayoletwa hospitalini, lakini baadaye wenzao wote hupotea na mgonjwa
kukosa wa kumhudumia, labda itokee bahati mbaya kwamba mgonjwa apoteze
maisha na ndipo hapo waliomleta na kumsaidia katika siku za awali
huonekana tena.
"Wengi wa vijana hawa ni wale ambao wanategemea
bodaboda kwa ajili ya kujipatia kipato. Wengine ni za kwao na wengine za
matajiri... hawa, wengi hutelekezwa na Moi hulazimika kuwagharimia,"
anasema Mvungi.
Mvungi anaelezea changamoto nyingine kuwa ni
kutelekezwa hospitali kwa majeruhi wa bodaboda. Anasema kundi la
waendesha pikipiki au watembea kwa miguu huokotwa kama wagonjwa
wasiofahamika na kwamba wanapofikishwa kwao, hutibiwa kwa matarajio kuwa
wakizinduka ndugu zao watajitokeza au wakipona watalipia gharama
wenyewe; lakini kwa baadhi yao hali huwa tofauti kwani hushindwa kulipia
kutokana na vipato vyao kuwa duni.
"Ni mzigo kwa taasisi
kumlisha mgonjwa, kumtunza na kumuwekea vifaa maalum ili arejee katika
hali yake ya kawaida. Lakini kupitia sera ya msamaha wa matibabu,
wagonjwa wa aina hii huwa wanasamehewa," anasema na kuwashauri madereva
wa bodaboda kujiunga na bima ya afya ili wanapopata ajali au kuugua iwe
rahisi zaidi kwao kupata matibabu.
MTAALAM WA USAFIRISHAJI ANENA Mkufunzi
wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Injinia Hans Mwaipopo, anasema vyanzo
vya ajali ni vitatu ambavyo ni binadamu anayechangia kwa asilimia 76,
chombo anachotumia asilimia 16 na mazingira asilimia nane.
Anasema
binadamu anachangi kwa asilimia hiyo kutokana na ukosefu wa elimu ya
usalama barabarani kwa vile wengi hawajui sheria zinazowaongoza wawapo
barabarani.
Mwaipopo anasema pia tabia ya kupuuza sheria kwa
wanaofahamu huchangia ongezeko la ajali; kuporomoka kwa maadili kwani
sasa ni rahisi mtu kupata cheti kwamba amesomea na kukionyesha hata kama
hajawahi kusomea udereva.
Aidha, Mwaipopo anaongeza kuwa lipo
pia tatizo la watu kupewa vyombo vya moto bila kujihakikishia kuwa ni
wazima kiakili kwani upo uwezekano kwa watu wenye matatizo ya akili
kuendesha vyombo vya moto kama pikipiki na hivyo kuhatarisha maisha ya
watu wasio na hatia.
Mkufunzi huyo anasema katika nchi nyingi
zilizoendelea, kabla ya mtu kukabidhiwa leseni anapimwa akili na hilo
pia linapaswa kuzingatiwa ili kupunguza ajali.
Mwaipopo
anasema sheria namba 30 ya 1973 na marekebisho yake inasema dereva
mwenye leseni halali anatakiwa kuwa na sifa kuu tatu, ambazo ni pamoja
na kusomea udereva katika chuo kilichosajiliwa na chenye walimu na macho
yake yawe yanaona vizuri.
Sifa nyingine ni kutokuwa na ulemavu
unaoweza kuathiri chombo cha moto anachoendesha, kuwa na akili timamu,
awe na afya njema na asiwe na maradhi yenye kuathiri chombo
anachoendesha kama ugonjwa wa moyo, sukari na kifafa.
" Leo hii
wapo madereva wana matatizo ya kifafa. Tukifanya ukaguzi, tutabaini
kwamba wapo wengi wana matatizo ya macho, kifafa, moyo na sukari lakini
wanaendesha vyombo vya moto. Hii ni hatari," anasema.
Anasema
chombo kinachangia kwa asilimia 16 kwa maana ya matumizi mabaya, ikiwa
ni pamoja na chombo kwisha muda wake wa matumizi, lakini bado
kinaendelea kubaki barabarani.
Anasema mazingira yanachangia kwa
asilimia nane, ikitokana na miundombinu mibovu na kukosekana kwa alama
muhimu katika barabara na pia barabara kulazimishwa kona pasipostahili
na nyingi kujengwa chini ya kiwango.
Anasema changamoto iliyopo
kwa watu wa bodaboda, ni tabia ya wengi wao kufundishana wao kwa wao.
Hawajifunzi sheria za usalama barabarani na hivyo hujiona wenye haki
kuliko watumiaji wengine.
"Mara kwa mara huwa tunawaona... mtu
anatakiwa kupita kushoto, yeye anapita kulia na hawana kofia ngumu...
katika hili hatuwezi kutafuta mchawi, ni lazima ajali zitaendelea
kutokea na vifo na majeruhi kuongezeka," anasema.
AJIRA NA FOLENI
Bodaboda
zimekuwa zikisaidia kupunguza tatizo la usafiri katika maeneo mengi
nchini. Katika maeneo ya mijini kama Dar es Salaam ambako tatizo la
foleni limekosa suluhu ya haraka, bodaboda ndiyo kimbilio.
Kwenye
maeneo yasiyofikika kirahisi kwa usafiri wa gari, hasa vijijini,
bodaboda pia zimetwaa nafasi. Vyombo hivi ni mkombozi pia wa Watanzania,
hasa vijana wanaokabiliwa na tatizo la ajira.
Dereva Sudi Hassan
wa Mbagala Charambe anasema kuwa kwa wastani, kila siku huwa hakosi
kuingiza Sh. 20,000, sawa na Sh. 600,000 kwa mwezi na kiasi hiki ni
kikubwa mno kulinganisha na wastani wa pato la Mtanzania kwa mwaka
(2013) ambalo ni Sh. 1,186,424, sawa na Sh. 98, 868.67 kwa mwezi, au Sh.
3,295.62 kwa siku; hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali
iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwenye Mkutano Mkuu wa 30 wa
Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) uliofanyika jijini Tanga Mei 14, 2014.
Hata
hivyo, vifo vya ajali za vyombo hivi vinavyosababisha kuongezeka kwa
idadi ya wajane na watoto yatima nchini huhalalisha hisia kwamba pamoja
na faida zake, bodaboda ni "muuaji wa kimyakimya".
Ajali za
bodaboda zimekuwa zikichangia ongezeko la yatima. Takwimu zilizowahi
kutolewa mwaka 2011 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto, zilionyesha kuwa Tanzania ilikuwa na watoto yatima
milioni 2.4 hadi kufikia mwaka 2011; kati yao wasichana wakiwa 1,055,000
na wavulana 1,345,000.
Aidha, ajali za bodaboda zinaathiri
uchumi wa watu mmoja mmoja na taifa. Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga, idadi
ya pikipiki zilizohusika katika ajali mwaka 2013 peke yake ni 8,241.
Hivyo, ikiwa kila pikipiki hununuliwa kwa wastani wa Sh. milioni 2 na
kisha kuharibika kabisa baada ya kupata ajali, maana yake jumla ya Sh.
bilioni 16.48 zilipotea katika kipindi cha mwaka 2013.
Kadhalika,
vipato vya watu wanaotegemea pikipiki hizo kwa shughuli za kibiashara
viliathirika kwa kiasi kikubwa kwani, kama kila dereva wa bodaboda
alitarajia kuingiza wastani wa Sh. 600,000 kwa mwezi (kama ilivyo kwa
dereva Hassan wa Mbagala Charambe), maana yake ni kwamba pato la jumla
ya Sh. 7,200,000 lilipotea kwa kila pikipiki kwa mwaka 2013.
Hivyo,
kwa taifa zima (pikipiki 8,242), kiasi kilichopotea kutokana na
bodaboda zilizohusika katika ajali ni Sh. bilioni 4.94. Kwa makadirio ya
jumla, hasara iliyotokana na gharama za kuharibika kwa pikipiki hizo
pamoja na kipato kilichopotea kwa kutokuwapo barabarani kwa pikipiki
hizo kwa mwaka wa 2013 ni takriban Sh. bilioni 21.
UZOEFU WA UGANDA
Changamoto
zitokanazo na ajali za bodaboda zipo pia katika nchi nyingine za
Afrika, Mashariki. Kwa mfano, nchini Uganda, mwaka 2011 pekee, madereva
wa bodaboda 570 walifariki dunia. Wodi ya dharura katika Hospitali ya
Rufaa ya Mulago jijini Kampala imepachikwa jina la "bodaboda" kutokana
na kuwa na majeruhi wengi wa ajali za bodaboda. Hospitali hii peke yake,
kwa mwaka hupokea wastani wa majeruhi 7,280, sawa na majeruhi 20 kwa
siku.
KAULI ZA MADEREVA
Frank Chungu aliyefanya
kazi ya kuendesha pikipiki kwa miaka mitano katika kijiwe cha Mwenge
jijini Dar es Salaam anasema chanzo cha ajali nyingi za bodaboda ni
matumizi ya vilevi kama bangi na pombe kali za kwenye vipakiti ambayo
hutumiwa na waendesha pikipiki wengi.
Anasema wengine hujifunza
kwa muda mfupi na kuingia barabarani kama madereva kamili na matokeo
yake, wengi kati ya hao hawafuati sheria za usalama barabarani na
kujiweka katika hatari kubwa ya kupata ajali.
"Wengi hawaheshimu
taa za barabarani, Wanapita upande ambao siyo sahihi. Hawako makini,
wanatumia pombe … na kuvuta bangi. Kwa hali kama hii ni lazima kutakuwa
na ongezeko la ajali," anasema.
Chungu anasema hivi sasa walau
kuna mabadiliko kidogo ukilinganisha na miaka michache iliyopita hasa
kutokana na wengi wa madereva kuingiwa woga baada ya kushuhudia wenzao
wengi wanavyojeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu na wengine kupoteza
maisha huku wakiacha wake na watoto zao.
Kuhusu leseni, anasema
kwa sasa wengi wao wana leseni, lakini tatizo ni kwamba, hawajifunzi kwa
umakini kwani wapo wanaokwenda kujifunza uwanjani siku ya kwanza na ya
pili yake wanaingia barabarani kupakia abiria.
Anasema wengine
huendesha kwa kasi kubwa kwa sababu tu ya kutaka wasifiwe kuwa wao ni
mahiri na kwa bahati mbaya, kadri pikipiki inavyozidishwa mwendo ndivyo
inavyokuwa nyepesi kuiendesha na hivyo dereva kusahau kuwa tofauti na
gari, wao wakipata ajali ni miili yao ndiyo hujigonga na hivyo kuwa
katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha au kuwa walemavu.
NINI CHA KUFANYA
Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mpinga, anasema kwa mujibu wa
sheria ya usalama barabarani, sura ya 168 kama iliyofanyiwa marekebisho
mwaka 2002, mtu yeyote, ili apate leseni ni lazima kwanza apate mafunzo
kwenye vyuo vya udereva.
Kuhusu madereva pikipiki anasema Chuo
cha Ufundi Stadi (Veta), wanaendesha programu ya mafunzo kwa madereva
pikipiki, lakini kinachosikitisha wengi hawapendi kwenda kujifunza.
Anasema
wengine wanaotoa mafunzo ni wadau mbalimbali wa masuala ya usalama
barabarani ambao hupita kwenye maeneo ya vijiwe vya madereva wa bodaboda
kwa ajili ya kufundisha matumizi ya pikipiki yanayozingatia usalama wa
waendeshaji wa vyombo hivyo na abiria wao.
Kutokana na kasi ya
utoaji wa mafunzo kwa sasa, kati ya waendesha pikipiki 700,000 waliopo
nchini kote, asilimia 70 tayari wamepata leseni.
Injinia Mwaipopo
anasema ni lazima serikali ichukue hatua madhubuti za kuwafundisha
waendesha pikipiki wote ambao wanategemea kazi hiyo kama ajira yao ya
kila siku katika kujiingizia kipato.
"Ukitaka kukamua jipu huwezi
kulikanda. Lazima ukamue usaha wote utoke, na ndiyo pona ya mgonjwa...
ajali nyingi, wengi hawajui sheria na hawataki kujifunza. Lazima
tuchukue hatua mapema vinginevyo idadi ya walemavu itaongezeka siku hadi
siku," anasema. CHANZO: NIPASHE