JAJI WARIOBA, NISINGEVUNJWA MOYO NA ‘MAMLUKI’ WA KISIASA

Jaji  Joseph Sindwe Warioba akitolewa nje ya ukumbi wa Ubungo Plaza jijini dar kwenye mdaharo wa kujadili umhimu wa wananchi kuitambua rasimu ya katiba, mdaharo uliokuwa umeandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere chini ya Mwenyekiti wake Joseph Butiku.
Kwako Jaji Joseph Sinde Warioba.Nakupa pole kwa misukosuko ya hapa na pale inayokupata, tangu ulipokabidhiwa na Rais jakaya Kikwete jukumu la kuongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Najua kwa sababu za usalama wako binafsi, itakuwa vigumu kwa mimi na wewe kukutana ili nikufikishie ujumbe wangu kwako. Kwa kuzingatia hilo, ngoja nikufikishie ujumbe kupitia safu hii.Mimi sikuzaliwa Septemba 3, 1940, Bunda mkoani Mara kama wewe. Nakuhakikishia kuwa sikusomea kwenye Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki na kuhitimu mwaka 1966. Sijawahi kuwa mwanasheria mkuu wa nchi hii kuanzia mwaka 1966 hadi 1968 kama wewe na sijawahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania kama wewe tangu mwaka 1985 hadi 1990, wala sina ndoto hizo.
Jaji  Joseph Warioba akinena.
Sijawahi kuwa waziri mkuu na makamu wa rais wa nchi hii kwa sababu sina sifa hata moja inayoweza kufanya nikashika wadhifa huo mkubwa katika nchi kama wewe. Sijawahi kuwa jaji katika Mahakama ya Sheria ya Afrika Mashariki wala sijawahi kuwa waziri wa sheria wa nchi hii.
Sikuteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuongoza tume maalum ya kupambana na rushwa kama wewe wala sijawahi kuwa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama wewe.
Sijui chochote kuhusu sheria, niponipo tu naganga njaa mjini, nazugazuga ilimradi mkono uende kinywani na maisha yasonge mbele. Hata hivyo, ningekuwa mimi kwenye nafasi  yako, kwa haya yanayoendelea kutokea hivi sasa, nakuapia kuwa kamwe nisingevunjwa moyo wala kukatishwa tamaa na mamluki wa kisiasa wanaokushambulia kila kukicha.
Ulipoteuliwa na Rais Kikwete kuongoza tume ya mabadiliko ya katiba, kila mmoja alikutazama kama tumaini la kweli la Tanzania ya kesho yenye ustawi katika kila sekta, kuanzia sheria, utawala bora mpaka maendeleo ya mwananchi mmojammoja kupitia katiba mpya ambayo wewe ndiye uliyepewa jukumu la kuzunguka kwa wananchi na kuwasikiliza maoni yao juu ya katiba wanayoitaka.
Walioamini hivyo hawakukosea kwani uliifanya kazi yako ipasavyo na kudhihirisha kwamba ‘mtu mzima dawa’.
Hata ulipokabidhi rasimu ya katiba hiyo kwa Rais Kikwete na kuiwasilisha kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa mujibu wa kifungu 20 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, kila mmoja alijua sasa mambo yatanyooka na Tanzania itajikwamua kutoka hapa ilipokwama kwa zaidi ya miaka 50 tangu uhuru.
Maskini! Haikuwa hivyo, bunge lilipoanza tu, kazi kubwa iliyotukuta uliyoifanya wewe na wajumbe wengine waliokuwa kwenye kamati yako, ilianza kubezwa na kupuuzwa, kashfa na maneno ya kuudhi yakaanza kutolewa, wakati mwingine yakikulenga moja kwa moja.
Ukaitwa majina mengi mabaya kwa sababu tu eti rasimu ya wananchi uliyoiandika ilionekana kuwa mwiba kwa vigogo wenye uchu wa madaraka, wasiotimiza ahadi zao kwa wanacnhi na wanaondekeza milungula na kujilimbikizia mali na kutupa maadili ya uongozi.
Wengine wakawa wanakuvukia mipaka bila kujali kwamba uelewa wako kwenye mambo ya sheria ni mkubwa na wa kipekee, wakasau kwamba kiumri pia wewe ni baba au babu yao. Wengine wakafikia mpaka hatua ya ‘kukuvuta sharubu’ hadharani.
Hata hivyo, mimi nikwambie kitu kimoja mheshimiwa! Hizo kelele wanazokupigia zinamaanisha kwamba wewe ni mti wenye matunda, lazima utapopolewa mawe tu mzee. Kamwe wasikukatishe tamaa kwa sababu wewe ni shujaa wa kweli wa nchi hii usiyeogopa kusema ukweli. Huku mtaani watu tunatamani hata ungekuwa bado kijana ugombee wewe urais ili uiokomboe nchi hii. Wasalaam.
JAJI WARIOBA, NISINGEVUNJWA MOYO NA ‘MAMLUKI’ WA KISIASA JAJI WARIOBA, NISINGEVUNJWA MOYO NA ‘MAMLUKI’ WA KISIASA Reviewed by Unknown on 12:18:00 AM Rating: 5
Powered by Blogger.