RISASI ZATUMIKA KUWATAWANYA WEZI WA MAFUTA YA PETROL WALIOVAMILA LORI LILILOPATA AJALI ENEO LA TABATA KISIWANI KWA MAMA PINDAPINDA.
Ilikuwa ni hekaheka, patashika nguo kuchanika, wakati risasi na mabomu ya machozi ziliporindima kutoka kwa Jeshi la Polisi kuwatawanya wananchi waliokuwa wakichota mafuta yaliyomwagika kutoka kwenye lori la mafuta aina ya scania lililopata ajali.
Sinema
ilianza saa tatu usiku wa kuamkia jana baada ya lori hilo lililobeba
shehena ya mafuta ya petroli, kushindwa kupanda mlima, kuserereka kisha
kupinduka, eneo la Tabata Kisiwani kwa Mama Pindapinda.
Baada
ya ajali hiyo, mafuta yalianza kumwagika na kuwavutia wakazi wa jirani
na eneo hilo waliobeba vyombo mbalimbali yakiwamo mabeseni na ndoo za
maji ili kuchota nishati hiyo.
Mjumbe wa Mtaa Bonde la Mchicha, Tabata Kisiwani, Mama Pindapinda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema
kwamba alipiga simu polisi kuwataarifu na walifika, lakini baada ya
gari hilo kuondolewa eneo la tukio, polisi nao waliondoka usiku wa saa
8.
Alieleza
kuwa na baada ya hapo, wakazi hao waliendelea kuchota mafuta na
kusababisha magari kushindwa kupita eneo hilo hali iliyosababisha mtaa
huo kufungwa kabisa.
Waendesha
bodaboda kutoka kila kona ya mitaa ya Tabata, walikusanyika na kujaa
eneo hilo ili kununua mafuta kwa bei nafuu na wengine kuamua kuvaa nguo
za kazi na kujichotea petroli hiyo.
“Nimeamka saa kumi usiku kuchota mafuta na nimeyauza ya Sh20,000,”alisema mwanamke mmoja aliyekuwa eneo hilo akiwa amelowa mafuta mwili mzima.
Hadi
kufikia saa 3 asubuhi, waendesha bodaboda waliendelea kumiminika eneo
hilo, wengi wakiwa na chupa kubwa za maji ya uhai, madumu ya lita 20 na
yenye ujazo wa lita tano wakisomba mafuta hayo.
Sehemu yalipomwagika mafuta hayo, yalionekana mashimo mfano wa visma, vilivyochimbwa na wakazi hao kwa ajili ya kupata mafuta.
Mtaa
huo na maeneo jirani, yalitawala harufu ya petroli, huku baadhi ya
wakazi wake wakiamua kuzima umeme na kutowasha moto kuhofia kutokea kwa
mlipuko.
Hata
hivyo, tafrija hiyo ya mafuta haikudumu kwa muda mrefu, kwani ilipofika
saa tano asubuhi, kundi la Jeshi la Polisi na Askari wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia(FFU), walifika eneo hilo na kuanza kuwatawanya wakazi
hao kwa risasi, ambapo walianza kukimbia huku na kule.
Risasi
hizo ziliwatawanya pia waendesha bodaboda walioanza kukimbia na vyombo
vilivyojaa mafuta, huku baadhi wakizitelekeza pikipiki zao.
Kutokana
na hali hiyo, polisi hao waliamua kuzichukua pikipiki zilizotelekezwa,
huku wakizivunja baadhi na kusababisha heka heka zaidi na hofu kutanda
eneo hilo.
Vurumai
hizo zilileta madhara hata kwa majirani wa lilipotokea tukio, kutokana
na risasi kuathiri nyumba zao kwa kuvunjika vioo na kusababisha nyufa
kwenye kuta za makazi yao.
“Risasi imeingia ndani, tena hapa ambapo mtoto huwa analala. Imevunja kioo na kuharibu kabisa dirisha, “ alisema Adam Kihiki mkazi wa eneo hilo.
Mpaka
saa 7 mchana jana, bado polisi walionekana kutanda eneo hilo ili
kuwazuia wananchi wa eneo hilo, ambao walionekana bado wana uchu wa
kuchota mafuta hayo yaliyomwagika baada ya gari lililobeba kupinduka.
RISASI ZATUMIKA KUWATAWANYA WEZI WA MAFUTA YA PETROL WALIOVAMILA LORI LILILOPATA AJALI ENEO LA TABATA KISIWANI KWA MAMA PINDAPINDA.
Reviewed by Unknown
on
11:58:00 PM
Rating: