RITA: MADUDU YA KINA SITTI MKIENDELEA KUYAFUMBIA MACHO TUTEGEMEE AIBU ZAIDI! KWENU


Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), bila shaka mko vizuri mnaendelea kusimamia jukumu zito katika taifa letu.Usajili, Ufilisi na Udhamini siyo kazi ndogo. Ni kazi inayohitaji umakini wa hali ya juu maana matokeo ya ufanisi wenu ndiyo majibu ya shughuli nyingi katika nchi.
Watu wakitaka kusafiri, kutambulika katika maeneo mbalimbali nyinyi lazima mhusike kutatua.
Mkitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima. Namshukuru Mungu naendelea na majukumu yangu kama kawaida.  Nimewakumbuka leo kupitia barua hii ili niweze kuwafikishia yaliyoko katika akili yangu ndogo.
Madhumuni ya barua hii kwanza kabisa ni kutaka kuwauliza, hivi mmewahi kuwaza kwamba kuna uwezekano mkubwa wa watu kufanya madudu ya kufoji vyeti kama anavyodaiwa kufanya mshindi wa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu?Kwa kuanzia eneo hilo, ni vyema basi chombo chenu kikafanya tathmini upya katika kuhakiki taarifa mbalimbali na kuweka mfumo mzuri wa kudhibiti mtu kufanya udanganyifu wa aina yoyote.
Msisubiri hadi yatokee ya kutokea ndiyo muanze kuchukua hatua.
Kupitia suala la Sitti ni dhahiri inaonesha kuna walakini kwenye ofisi yenu. Haiwezekani nyaraka nyingine za mtu huyohuyo mmoja zioneshe kwamba amezaliwa mwaka 1989 huku mwenyewe akidai kuwa amezaliwa mwaka 1991.
Kinachonisikitisha zaidi mhusika anadai eti cheti chake cha kuzaliwa kilipotea na akadai kuwa mmempatia kingine kipya Septemba 9, mwaka huu.Alipoulizwa kwamba alitoa taarifa katika kituo gani cha polisi juu ya upotevu wa cheti chake hakuwa na jibu la kueleweka, mlimpaje?
Wakati umri wa mrembo huyo ukiendelea kuwa gumzo kwa takriban mwezi mzima, RITA mliendelea kuziba mdomo katika kung’amua umri halisi wa binti huyo licha ya wadau mbalimbali kuhoji juu ya hilo. Mtendaji Mkuu wa RITA, Jumamosi iliyopita alikaririwa katika chombo cha habari akisema bado wanaendelea kumchunguza miss huyo. Hadi lini?
Labda sina uzoefu juu ya mambo ya uchunguzi lakini kweli mfumo mlionao si rafiki kiasi cha suala hilo kuchunguzwa kwa zaidi ya wiki tatu? Nafikiri kuna haja ya kwenda mbele zaidi ya hapo. Dunia ya leo kila kitu kinakwenda katika mfumo ‘data base’ kwenye kompyuta.
Kwa nchi za wenzetu ni rahisi tu mtu kupata taarifa zake, tena hakuna kificho ndiyo maana utata wa Sitti ulipokuwa ukiendelea, watu ‘wali-google’ tu na kupata taarifa zote za Sitti kule Texas, Marekani na kila kitu kikawekwa hadharani. Kuanzia leseni ya udereva hadi hati ya kusafiria.
Ni wakati sasa umefika tubadilike, tutengeneze mfumo wa kuweka wazi data. Isichukue muda mrefu kubaini taarifa za mtu hususan katika suala la utaifa kama la Miss Tanzania ambaye anatakiwa akaiwakilishe nchi katika mashindano ya urembo ya dunia.
Wasalaam,
Erick Evarist.
RITA: MADUDU YA KINA SITTI MKIENDELEA KUYAFUMBIA MACHO TUTEGEMEE AIBU ZAIDI! KWENU RITA: MADUDU YA KINA SITTI MKIENDELEA KUYAFUMBIA MACHO TUTEGEMEE AIBU ZAIDI! KWENU Reviewed by Unknown on 11:46:00 AM Rating: 5
Powered by Blogger.