Roho mkononi! Jumla ya magari saba
yakiwemo mabasi mawili yaliyokuwa yakitokea jijini Dar es Salaam
kuelekea Mwanza, yametekwa na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi usiku wa
kuamkia Jumamosi ya wiki iliyopita, saa 6:30 usiku eneo la Ng’ungumalwa
mkoani Mwanza.
Polisi wakiwa eneo la tukio.
Miongoni mwa magari yaliyotekwa, mawili
yalikuwa ni mabasi ya abiria, Super Najmnisa na Princess Mnaa huku
mengine yakiwa ni malori na gari dogo moja ambapo inaelezwa kuwa
watekaji walitegesha mawe makubwa barabarani kabla ya kutekeleza tukio
hilo.
Wakizungumza na mwandishi wetu
aliyekuwepo eneo la tukio, baadhi ya madereva wa magari yaliyotekwa
walieleza kwamba walipofika eneo hilo, walikuta mawe yakiwa yametegeshwa
barabarani huku kukiwa na kundi la watu wenye silaha za aina mbalimbali
yakiwemo mapanga, marungu na bunduki.
Baadhi ya abiria waliotekwa.
“Walitushusha kwenye magari na kututaka
tusalimishe kila kitu tulichokuwa nacho zikiwemo fedha na simu za
mkononi. Waliokuwa wakionesha ukaidi walikuwa wakipigwa na kujeruhiwa
vibaya,” alisema dereva mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Madereva hao waliendelea kueleza kuwa
kazi hiyo ya utekaji iliendelea kwa takribani saa nzima ambapo kila gari
lililokuwa likija eneo hilo, lilikuwa likitekwa na watu kulazimishwa
kushuka chini na kutoa kila walichokuwa nacho.
Msichana huyu alizimia baada ya kutekwa.
“Walikuwa na mifuko mikubwa miwili,
mmoja ulijaa simu walizotupora na mwingine ulijaa fedha, kwa kweli
lilikuwa ni tukio baya sana, wengi walijeruhiwa vibaya,” alisema dereva
mwingine ambaye naye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Abiria wengine waliozungumza na Uwazi,
walienda mbele zaidi kwa kueleza kuwa mbali na kupigwa na kuporwa, pia
baadhi ya abiria wanawake walibakwa na kusababishiwa maumivu makali.
“Huu unyama tuliyofanyiwa wa kupigwa na
kuporwa mali zetu huku baadhi yetu wakibakwa unatisha sana na unaonesha
ni kwa jinsi gani nchi inaelekea kubaya, hakuna amani hasa katika
kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya,” alisema
mwanamke mmoja aliyekuwa miongoni mwa waliotekwa, aliyejitambulisha kwa
jina moja la Sara.
...Abiria wakiwa wameduwaa
Abiria hao waliliambia Uwazi kwamba eneo
hilo lina pori kubwa ambapo panahitajika doria za mara kwa mara za
polisi kwani ni eneo ambalo limekuwa maficho ya majambazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Valentino Mlowola alipopigiwa simu na kuulizwa juu ya tukio hilo,
alikiri kuwa na taarifa na kueleza kuwa polisi walifika katika eneo la
tukio muda mfupi baadaye baada ya kupata taarifa na kufungua barabara
iliyokuwa imefungwa na kuruhusu magari kupita.“Msako mkali unaendelea
kuwatafuta watuhumiwa katika Wilaya ya Kishapu na Kwimba,” alisema
Kamanda Mlowola.
MSIMU WA SIKUKUU ROHO MKONONI MABASI YATEKWA, WANAWAKE WABAKWA
Reviewed by Unknown
on
12:15:00 AM
Rating: