Dar es Salaam. Watu waliopokea mgawo wa fedha zilizochotwa kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huenda wakalazimika kulipa mamilioni ya Shilingi ambayo ni kodi ya mapato ya fedha walizopewa, imefahamika.
Hata hivyo, habari zinasema malipo hayo ya kodi yatafanywa kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya dola ambao unawashirikisha maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu uhalali wa fedha walizolipwa.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema juzi kuwa wote waliopokea mgawo wa fedha zilizochotwa kutoka katika akaunti hiyo watapewa fomu za kuthibitisha mapato yao ili wakatwe kodi kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa kuhakikiwa na vyombo vya usalama kwamba ni mapato halali.
Alisema taratibu za kufuatilia fedha hizo zimekwishaanza na ifikapo Desemba 31 wahusika watapewa fomu ili kuthibitisha mapato yao ili hatua za kuwatoza kodi zianze.
Msingi wa maelezo ya Nchemba umejengwa kwenye Sheria ya Mapato ya Kodi (Income Tax Act) ya 2012 ambayo inaelekeza mlipaji wa kodi kuwasilisha ankara za hesabu za mapato yake kwa TRA kila ifikapo mwisho wa mwaka na hesabu hizo huiwezesha mamlaka hiyo kutathmini kiwango cha kodi inayopaswa kulipwa na mhusika.
“Hotuba ya Rais (Jakaya Kikwete) imetupa nguvu kuendelea na juhudi ambazo tayari tulikwishazianza tangu awali, maana amesisitiza kwamba lazima kodi ilipwe na sisi hilo ni jukumu letu, tutafuatilia ili kuhakikisha kwamba fedha za walipakodi zinarejeshwa,” alisema Nchemba.
Ikiwa wote waliotajwa watalazimika kukatwa asilimia 30 ya fedha walizopewa kama kodi ya mapato, TRA itakusanya zaidi ya Sh9.3 bilioni ambazo zinatokana na karibu Sh31 bilioni zilizotawanywa kwa watu na kampuni mbalimbali kutoka kwenye akaunti ya mmiliki wa VIP Engineering, James Rugemalira.
Miongoni mwa waliokiri kupokea fedha hizo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye alipata mgawo wa Sh1.6 bilioni akisema fedha hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Hata hivyo, hatua yake hiyo tayari imemgharimu baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uwaziri wake kutokana na kile alichokiita kuwapo kwa makosa ya kimaadili hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti yake binafsi.
Taarifa ya PAC
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiwasilisha taarifa yake bungeni kuhusu suala hilo mwezi uliopita, pia iliwataja wengine waliochukua fedha hizo kutoka VIP Engineering kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni), aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh40.4 milioni) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni).
Wengine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni), Majaji wa Mahakama Kuu, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji Aloysius K Mujulizi (Sh40.4 milioni) pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni).
JE WAJUA,? WALIOPATA MGAWO WA ESCROW MAMBO HYA NDIYO YATAKAYP WATOKEA..
Reviewed by Unknown
on
8:24:00 AM
Rating: