MTU Aliyesadikiwa Kuwa na Ugonjwa wa Ebola Sengerema Mwanza, Azikwa kwa Taadhari Kubwa


MTU aliyesadikiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola Wilaya Sengerema mkoani Mwanza, amezikwa kwa hadhari kubwa na wataalamu wa afya.

Wakati mtu huyo akizikwa jana, hofu kubwa imetanda  mikoa ya Kanda ya ziwa, huku watu wakiogopa kugusana katika vyombo vya usafiri na kutumiana ujumbe mfupi wa simu za mikononi (SMS) juu ya kuchukua hadhari ya ugonjwa huo.

Mgonjwa anayedaiwa kufariki dunia kwa ugonjwa huo, ametajwa kuwa ni Salome Richad (17), mkazi wa Kahunda Wilaya ya Sengerema.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mganga Mkuu wa Hospitali Teule ya Sengerema, Mary Jose alisema mwili huo umezikwa na wataalamu ikiwa ni hatua ya kuchukua hadhari.

“Hakuna Ebola Sengerema, kilichofanyika ni hadhari tu, hii ni hadhari..narudia hakuna ebola Sengereama, kilichofanyika ni hadhari tu,” alisema.

Hata hivyo, Jose hakutaka kuzungumza zaidi kwa kile alichodai mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo ni Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO).

Wakimbiana kwenye daladala

Kutokana na hofu ya ugonjwa huo, jana wananchi walihaha katika vyombo vya usafiri hususan daladala, wakikataa kugusana.

Hali hiyo, ilisababisha wengi kuanza kutuma ujumbe mfupi kwa ndugu na jamaa kupitia simu za kiganjani kuwataarifu kutopeana mikono na mtu yeyote kwa kuwa Ebola imeingia Mwanza.

Imeelezwa hofu kubwa ipo katika Wilaya ya Sengerema ambayo inaonekana kuathirika zaidi.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Caren Yunus amewataka wananchi kuwa watulivu  kwa sababu ugonjwa huo bado haujathibitishwa rasmi.

Alisema sampuli zimechukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

Yunus aliliambia gazeti  hili kuwa, amesikitishwa na taarifa zinazodai Richard amekufa kwa ugonjwa wa Ebola baada ya kufikishwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema.

“Binafsi nasikitishwa na aliyetoa taarifa za Richard kwamba amefariki dunia kwa ugonjwa wa ebola… amepata wapi mamlaka ya kuzungumzia suala hili katika vyombo vya habari, uchunguzi kuhusu kifo cha binti huyo unaendelea na kwa taarifa za awali nilizonazo hakufariki kwa ugonjwa huo.

“Hivi sasa wananchi wamekuwa na hofu kubwa, sasa kama mkuu wa wilaya tunawahoji wale wote waliozungumza kwenye taarifa zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari tujue wapi walithibitisha wakati sampuli bado zipo Muhimbili,” alihoji.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Valentino Bangi, hajatoa kauli yoyote licha ya kutafutwa na waandishi bila mafanikio huku simu yake ikiita bila kupokelewa.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk. Rutachunzibwa Thomas alisema amesikia taarifa ambazo si rasmi za kifo cha mtu mmoja anayedaiwa kuwa na dalili za Ebola na kuwataka wananchi mkoani humo kuchukua hadhari kutokana na ugonjwa huo hatari.

Alisema wananchi wote bila ya kujali mtu yuko kwenye nafasi gani, anapaswa kuchukua tahadhari na kuwaelimisha wananchi juu ya dalili za ugonjwa huo, ambao haujapata dawa.

“Ninaloweza kusema ni kwamba, ugonjwa huu tusiwaachie watu wanaofanya shughuli za sekta ya afya, bali kila mtu atoe ushirikiano kuanzia ngazi ya kaya kwa kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono na kukumbatiana, pia ikiwa kuna mtu atabainika kuwa nao ni vema tahadhari ikachukuliwa maana ukigusa damu yake, jasho na mambo mengine unaupata.

“Mpaka sasa ugonjwa huo umetajwa katika wilaya iliyopo jirani na mpaka wa Uganda na Tanzania, ila sina taarifa za ugonjwa kuingia mkoani Kagera,tunachukua hadhari zote,” alisema Dk. Thomas.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya watu waliofariki na ugonjwa wa Ebola imefikia 1,350 na idadi hiyo inaweza kuongezeka katika siku za hivi karibuni kutokana na kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali duniani.

Taarifa hii imeandaliwa na Benjamin Masese, John Maduhu (Mwanza), Shomari Binda (Mara) na Renata Kipaka (Kagera).
MTU Aliyesadikiwa Kuwa na Ugonjwa wa Ebola Sengerema Mwanza, Azikwa kwa Taadhari Kubwa MTU Aliyesadikiwa Kuwa na Ugonjwa wa Ebola Sengerema Mwanza, Azikwa kwa Taadhari Kubwa Reviewed by Unknown on 12:52:00 AM Rating: 5
Powered by Blogger.