NASIB Abdul, ambaye uwezo wake wa muziki wa kizazi kipya umempatia jina la Diamond
Platnumz, mwishoni mwa wiki iliyopita katika tamasha la Fiesta, pale
Leaders Club Kinondoni jijini Dar es Salaam, itabaki kuwa ndani ya
kumbukumbu zake, angalau kwa miaka kadhaa ijayo.
Mamia ya mashabiki waliojazana katika viwanja hivyo, walimzomea kwa
nguvu kubwa, tofauti na matarajio ya wengi kwamba angefunika, kama
wenyewe wanavyosema. Kelele zile za kuzomewa zilimshtua hadi Diamond mwenyewe, ambaye alikiri jukwaani pale kwamba haikuwa bure, lazima kulikuwa na kitu.
Baada ya tukio lile, watu wameongea mengi sana, ikiwa ni pamoja na
propaganda kwamba zomeazomea ile ilipangwa. Na nani? Hapo ndipo penye
kizungumkuti. Wengine wanasema eti mashabiki wa Ali Kiba ndiyo walipanga
ili kumuonyesha kwamba yeye hakuwa bora zaidi ya msanii wao.
Wengine wanasema watu f’lanf’lan (wanawataja majina) ndiyo hasa walikuwa
nyuma ya zoezi lile, eti walikodi watu na kuwalipia ili wahakikishe Diamond
Platinumz hakamati shoo. Sababu, eti kadiri anavyokuwa juu, bei yake ya
kukodishwa inapanda na hivyo kuwapa taabu watu kumtumia katika ishu
zao.
Bahati mbaya sana, Babu Tale, ambaye tunamtambua kama Meneja wake, naye
ameingia kwenye kundi hili la kuamini kuwa zomeazomea ile ilipangwa kwa
sababu zilizotajwa hapo juu. Anadai eti kupata taarifa za kuwepo kwa
tukio hilo mapema.
Binafsi, siamini kama Ali Kiba au mtu mwingine yeyote alihusika
kuwaambia mashabiki wamzomee, isipokuwa Diamond mwenyewe alijitengenezea
mazingira ya kuzomewa. Zipo sababu kadhaa zinazoweza kuchangia jambo
hili kutokea, lakini kubwa ninaloliona, ni tabia.
Hatuwezi kufanana tabia hata siku moja, lakini angalau zipo tabia ambazo mtu unapaswa kujitahidi kuzionyesha mbele ya watu wanaokuzunguka.
Hatuwezi kufanana tabia hata siku moja, lakini angalau zipo tabia ambazo mtu unapaswa kujitahidi kuzionyesha mbele ya watu wanaokuzunguka.
Diamond amelewa umaarufu kiasi kwamba anadhani yupo juu ya kila mtu, kwa
sababu anachokifanya mbele za watu ni maisha ya kuigiza, yaani yasiyo
ya Kitanzania hasa.Katika kipindi cha muda mfupi, aliwapa zawadi ya
magari mama yake mzazi pamoja na mpenzi wake, Wema Sepetu wakati
wakisherehekea kumbukumbu ya siku zao za kuzaliwa. Siku za nyuma
niliwahi kumsikia katika televisheni moja akidai ana shilingi bilioni
moja benki.
Siyo jambo baya kumpa mama na mpenzi wako zawadi ya gari, lakini una
sababu gani ya kuita kamera? Halafu, kama Diamond mwenye miaka mitano ya
umaarufu ana fedha kiasi hicho, Profesa Jay, AY, Lady Jaydee, FA na
Juma Nature ambao wamekuwa juu miaka zaidi ya kumi mfululizo, wana
shilingi ngapi benki?
Kwamba wao hawaandai bethidei, hawana wapenzi au hawajui kujipromoti?
Diamond amehama kutoka katika maisha yake ya asili na sasa anataka
kuishi kama akina P. Diddy. Anachokosea, kwa maoni yangu, ni
kujitangaza, lakini vinginevyo angeweza kufanya hayo anayoyafanya lakini
kimyakimya.
Wabongo hawapendi mtu wa hivyo, hasa wanayemjua vizuri ujio wake kama Diamond. Zomeazomea hii ni ishara kwake kwamba abadili aina ya maisha anayoishi.
Wabongo hawapendi mtu wa hivyo, hasa wanayemjua vizuri ujio wake kama Diamond. Zomeazomea hii ni ishara kwake kwamba abadili aina ya maisha anayoishi.
Mimi bado nina imani kubwa na uwezo wake katika jukwaa. Wala zomea ile
isimkatishe tamaa, bali kama nilivyosema, abadilike kidogo tu. Ajiulize
kwa nini Nature akipanda jukwaani Temeke nzima inalipuka, ajiulize kwa
nini Jay bado kinara licha miaka kibao ya usupastaa?
Ni kwa sababu wanaishi maisha ya watu wao. Ni kweli kwamba hawezi kukaa
katika vijiwe vya zamani, lakini basi asisahau lugha yao. Akikutana nao
aseme nao, siyo kila siku kuonekana mtu wa warembo na matanuzi mengine
ambayo kwa tafsiri rahisi za wabongo, ni kuwa anajiona, ana nyodo!
Mimi kwetu kijijini, kuna watu hawajawahi kufika Dar es Salaam, lakini
nikienda kule, nazungumza lugha yao, kana kwamba na mimi sijawahi
kufika. Ninapolazimika kuongea kuhusu Dar, basi ni vile vitu ambavyo wao
wangependa kuvisikia. Na kumbuka, nikihitaji kupata kiburudisho,
ninakunywa kinywaji ambacho kinanywewa na nao, kwani hatari kitu gani?
DIAMOND, KUNA KITU CHA KUJIFUNZA
Reviewed by Unknown
on
11:16:00 PM
Rating: