Taasisi Ya Kiislam Yatishia Kuandamana Nchi Nzima......Yaipa Serikali Siku 15 Kufungua Madrasa na Kuwaachia Huru Masheikh Waliokamatwa

Jumuiya na Taasisi za Kiisalam nchini, imetoa tamko na kuipa serikali siku 15 kabla ya kufanya maandamano nchi nzima kuelekea Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakidai kufunguliwa kwa madrasa zilizofungiwa kwa kuhusishwa na kutoa mafunzo ya ugaidi.

Masharti mengine ni kuachiliwa huru au kwa dhamana masheikh na maimamu waliokamatwa wakituhumiwa kutoa mafunzo na mazoezi ya kigaidi.

Maeneo ambayo madrasa hizo zaidi ya 10 zimefungwa ni katika mikoa ya Kilimajaro, Dodoma na Mtwara. Tamko hilo pia lilisema jeshi hilo linawatuhumu kwa kukusanya watoto na kuwafundisha elimu ya dini katika mazingira yasiyofaa na kuwapo kwa taarifa za watu wenye milipuko misikitini na kujihusisha na ugaidi.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sheikh Musa Kundecha, alisema jeshi hilo limekuwa likiwakamata watu hao usiku na kuwapeleka katika vituo vya polisi, na kuwahoji.

Alisema jeshi hilo limekuwa likifanya kazi za maofisa wa ustawi wa jamii na elimu, kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo watoto hao wanafundushwa elimu ya dini ya kiislamu.

“Mkakati wa operesheni hii unakiuka utu, haki za binadamu, kikatiba na ni uchochezi dhidi ya Waislamu kuwafanya wachukiwe na jamii, tunawatunza yatima katika maeneo jirani na madrasa na kuwapa elimu ya kidini siyo kosa, tunatimiza wajibu wa kidini. Wajibu wa serikali ni kutulinda, lakini tunawekwa katika mazingira ya hatari,” alisema Kundecha.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, alisema ulifanikiwa utafiti, kabla ya jeshi hilo kuchukua hatua za kufunga baadhi ya madrasa na kuwakamata watu hao.

“Katika maeneo ya mikoa hiyo ni kweli kuna suala hilo, na watoto ambao wana umri wa kuwa shule walikutwa pale, hivyo tukataka kufahamu na yajulikane mafunzo wanayopewa,” alisema Nantanga.

Alisema kuendelea kushikiliwa kwa baadhi ya watu waliokamatwa na kunyimwa dhamana kunatokana na jeshi hilo kutojiridhisha au kutokamilika kwa taratibu za dhamana.

“Pale mtuhumiwa atakapoachiwa, ni lazima polisi wajiridhishe kabla ya kumpatia dhamana mtuhumiwa. Hadi hivi sasa, kama wizara hatujapokea tamko lolote kuhusu jambo hili, tunasubiri kupokea rasmi tamko, na tutaliweka mezani na kulifanyia kazi,” aliongeza.
Taasisi Ya Kiislam Yatishia Kuandamana Nchi Nzima......Yaipa Serikali Siku 15 Kufungua Madrasa na Kuwaachia Huru Masheikh Waliokamatwa  Taasisi Ya Kiislam Yatishia Kuandamana Nchi Nzima......Yaipa Serikali Siku 15 Kufungua Madrasa na Kuwaachia Huru Masheikh Waliokamatwa Reviewed by Unknown on 12:58:00 PM Rating: 5
Powered by Blogger.